Ruka hadi kwenye maudhui makuu

SOMO: MAONO NA NDOTO


MAONO NA NDOTO * sehemu ya nane & na ya mwisho *

Bwana Yesu asifiwe…
02.NDOTO
maono 03
Ingawa ndoto nyingi zinazo-otwa huwa hazina maana Lakini zipo baadhi ya ndoto zenye maana na zenye kubeba ujumbe mkubwa.
Katika maandiko matakatifu,Biblia ;Zipo ndoto nyingi ambazo Bwana Mungu alikuwa akisema na watu wake tofauti tofauti katika muda tofauti tofauti.
Kulikuwa na wakati ambapo Bwana Mungu alipotaka kuwaonya watu wake,au pale alipotaka kuwapa maelekezo juu ya mambo yajayo alitumia njia ya NDOTO.
Hivyo;
Ndoto ikawa mojawapo ya njia ya mawasiliano baina ya Mungu na watu wake.
Jambo moja la msingi ambalo tunapaswa kujua siku ya leo ni hili;
*Uotapo ndoto yoyote usimwambie mtu yeyote Bali umuulize Bwana Mungu kwanza.
Haleluya…
Si kila mtu utakaye mshirikisha ndoto yako,atakuunga mkono wengine wataifisha hiyo ndoto. Yamkini Mungu amesema na wewe kwa njia ya ndoto,ujumbe huo ambao Bwana Mungu ameuachilia kwako una kuhusu wewe na Yeye kwanza,ndio maana mwingine amefichwa ila kwako limefichuliwa kwa ndoto.
Sasa ukienda kumuuliza mwanadamu,mwanadamu awaye yote hawezi kukujibu maana yeye mwenye mwili naye humuitaji BWANA MUNGU.
Ndiposa ninakuambia USIJE UKAANZA KUOMBA MSAADA KWA MWANADAMU KABLA YA KUMUOMBA MUNGU.
Maana ukiona wewe umepewa fursa ya kupata ndoto yenye ujumbe kamili basi ujue ni wewe ndio uliyekusudiwa ujumbe huo ili hufanyie kazi ndoto hiyo,na yamkini kupitia wewe ujumbe ukamilike.
Zingatia hili;
Sisemi usimshirikishe kabisa mtu,hapana!
Kwanza wa kuombwa majibu ya ndoto ni Mungu kisha ikiwa umeomba mbele za Bwana Mungu na hukupata majibu ya ndoto uliyoota ndiposa waweza ukamwendea mtu mwenye karama ya kufasiri ndoto,kwa huyo mtu wa Mungu aweza kukusaidia kuomba kwa Mungu na hatimaye Mungu akakufunulia hiyo ndoto yako.
Nimekwambia si wote watafurahia ndoto yako maana wengine watajaribu hata kuiua.
Tunamjua mtu mmoja aitwaye Yusufu.Alipoota tu akaenda kuwaambia watu ndugu zake. Ndugu zake wakamchukia hata kutaka kumuua.
Yusufu akaota ndoto,akawapa ndugu zake habari,nao wakazidi kumchukia; ” Mwanzo 37:5
Biblia inasema kwamba ndugu zake Yusufu wakamchukia Yusufu.Hawa ndugu hawakumchukia Yusufu kwa mambo mengine yoyote,isipokuwa walimchukia kwa sababu ya NDOTO alizoziota Yusufu.
Hatuoni Yusufu akimuuliza Bwana Mungu ili apewe maelekezo sahihi ya kile alichokiota,Bali tunachokiona ni kwamba mara Yusufu alipoota tu,akaenda moja kwa moja na kuwapasha habari ndugu zake.
Ndugu zake wakamchukia yeye kwanza,na wala hawakuchukia ndoto aliyoota. Baadaye tunaona wakataka kumuangamiza kwa sababu ya kile alichokiota.
Vivyo hivyo kwako mpendwa;
Waweza kuoto ndoto kubwa sana,na ukijaribu kwenda kuwashirikisha wanadamu pasipo kuanza na Mungu ujue hao wanadamu watakuchukia wewe na wala hawataichukia hiyo ndoto.
Haleluya…
Bwana Yesu asifiwe….
Nazungumza na mtu mmoja mahali hapa,
Bwana wa Bwana anastahili sifa….
Biblia inazidi kueleza kwamba Yusufu akaota ndoto nyingine. Ndoto nyingine aliyoiota Yusufu ilikuwa inafanana na ile ndoto ya kwanza aliyoiota.
Ukisoma Mwanzo 37:7-8 utakuta Yusufu akiwaeleza ndugu zake ndoto ya kwanza aliyoiota,lakini pia ukisoma Mwanzo 37:9-11 utakuta Yusufu yule yule akiwaeleza ndugu zake ndoto ya pili aliyoiota.
Ukilinganisha ndoto hizi mbili utangua kwamba;
DHIMA yake inafanana ingawa mahitaji yaliyotumika yalitofautiana.
Dhima ni ujumbe wa msingi.Ujumbe katika ndoto hizi mbili ulifanana.
Mahitaji ni vibebea ndoto ili dhima ikamilike. Mfano wa mahitaji/requirements ya ndoto ya kwanza yalikuwa ni MIGANDA wakati ndoto ya pili ilikuwa ni JUA,MWEZI na NYOTA.
Haleluya….
Nasema,Haleluya…
Jambo la pili tunalojifunza hapo ni kwamba;
*Ndoto yenye kubeba ujumbe mkubwa wa ki-Mungu,mara nyingi NDOTO hujirudia zaidi ya mara moja.
Ujumbe ambao Yusufu alioneshwa katika ndoto ulikuwa ni ujumbe mkubwa sana kiasi kwamba tunaona BWANA MUNGU akijaribu kumuelezea Yusufu mara mbili kwa jambo lile lile.
Leo;
Ukiona una ndoto yenye kupata kujirudia rudia hujue lipo kusudi la msingi ndani ya ndoto hiyo,tena usije ukaipuuzia hata kidogo.
Sisemi kwamba ni lazima ndoto yenye kusudi ijirudie rudie.Zipo baadhi za ndoto zenye maana kamili ambazo hujitokeza mara moja tu.Lakini nyingi hujirudia rudia kuonesha ya kwamba ipo kazi ya kufanya ndani ya ndoto za namna hizo.
Bwana Yesu asifiwe…
Biblia inazidi kueleza kwa habari ya ndoto ya Yusufu,kwamba;
“Ndugu zake wakamhusudu;bali baba yake akalihifadhi neno hili.”Mwanzo 37:11
Wapo wachache wenye kulihifadhi neno lako ulisemalo katika ndoto uliyoiota.Nasema watu wa namna hii wenye kuhifadhi ndoto yako ni wachache sana katika ulimwengu huu.
Watu weliopewa kulihifadhi neno usemalo,ni wale ulioambatana nao kiroho.Biblia inamuelezea vizuri sana mzee Yakobo jinsi alivyo ambatana na Yusufu kijana wake mdogo aliyempata enzi ya uzee wake.(Mwanzo 37 :3)
Mfano mzuri wa muambatano wa kiroho ni Elisabeth na Mariamu
Tazama pale Mariamu alipomwendea Elisabeth;
Biblia inasema ;
Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu,kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake;Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu;”Luka 1:41
Haleluya…
Kulikuwa na muunganiko mkubwa wa kiroho baina ya nguvu ya Mungu iliyokuwapo ndani ya tumbo la Mariamu na nguvu iliyokuwapo ndani ya tumbo la Elisabeti.Huu ni mfano mmojawapo wa muunganiko wa kiroho wa kipekee/A very completely spiritual bond.
Muunganiko kama huu ndio ulimfanya Yakobo aweze kutunza neno la Yusufu kwa kile ambacho Yusufu alichokiota.

MAONO NA NDOTO * sehemu ya mwisho *
NDOTO.
Wapo watu chini ya jua hili huitwa ”waota ndoto”.Watu wa namna hii wamepewa kuona mambo fulani katika ndoto.
Mfano;
Mtu mmoja alinijia na kuniambia; ” …mtumishi niliota ndoto,nikaona watu kama majambazi wameingia nyumbani kwangu na kuanza kuiba,…kisha nilipoamka asubuhi baada ya ile ndoto,yaani ile natoka nje tu,gafla nikakutana na umati wa majirani zangu ambao wengine walikuwa wakilia kwa ajili yangu.
Maana walidhani nimeuwawa usiku ule sababu kulikuwa na majambazi kweli ambao waliingia ndani ya chumba changu cha kulala wakiwa na silaha na nondo kadhaa mikononi mwao.
Khaa!
Kumbe kile nilichokuwa nakiota usiku kumbe ilikuwa ni tukio halisi lililokuwa likiendelea huku mimi naota tukio hilo hilo.
Majirani zangu wakaanza kunishangaa kwamba mimi ni mzima lakini nilipoingia ndani nikagundua waliniibia baadhi ya vitu vyangu vya thamani….
lakini tazama mtumishi,kile nilichokuwa nakiota ndicho kilikuwa kinafanyika muda ule ule…”
Hayo yalikuwa ni maneno ya mpendwa mmoja aliyekuwa akinisimulia.
Haleluya….
Jina la Bwana libarikiwe…
Mtumishi gasper 01
Mtumishi Gasper Madumla nikiwajibika madhabahuni.
Hivyo wapo watu wenye uwezo wa kuona tukio lenye kutukia wakiwa ndotoni.
Nami nakuambia usiipuzie ndoto uotazo.
Siku ya leo tutajifunza fundisho hili kupitia ndoto moja ndogo lakini ndio ndoto ngumu iliyopata kuandikwa katika Biblia.
Ndani ya Biblia tuisomayo kila siku,zipo ndoto mbali mbali,Lakini ipo ndoto moja yenye kuonekana ndogo lakini ndio ndoto ngumu kuliko zote.
Tunasoma:
Hata katika mwaka wa pili wa Kumiliki kwake Nebukadreza,Nebukadreza aliota ndoto;na roho yake ikafadhaika,usingizi wake ukamwacha.
Ndipo mfalme akatoa amri kuwaita waganga,na wachawi,na wasihiri na Wakaldayo,wapate kumweleza mfalme ndoto zake.Basi wakaingia,wakasimama mbele ya mfalme.
Mfalme akajibu,akawaambia Wakaldayo,Neno lenyewe limeniondoka;msiponijulisha ile ndoto na tafsiri yake,mtakatwa vipande na nyumba zenu zitafanywa jaa.” Danieli 2:1-2 & 5
Biblia imeeleza kuwa Nebukadreza,alipoota ndoto ile,usingizi wake ulimwacha kwa lugha nyingine hakupata usingizi kwa sababu roho yake ilifadhaika.
Alichokihitaji Nebukadreza ni kupata tafsiri sahihi ya ndoto yake pasipo kudanganywa.Yeye mwenyewe hakuwa na uwezo wa kufasiri hiyo ndoto,Ndiposa akawaita wachawi,waganga,wasihiri,na Wakaldayo.
Haleluya..
Wachawi,waganga na wasihiri walikuwa na mtihani mkubwa sana sababu uwepo wa maisha yao ulitegemea kuweza kutafsiri ndoto kwa usahihi,la sivyo maisha yao yapo hatarini.Hata hivyo hawakuweza kutafsiri ndoto ya mfalme.
Ndoto hii imekuwa ni ndoto ngumu kutafsiriwa sababu kile kilichokuwa kimeotwa kimesahaulika,Nebukadreza anasema;
…Neno lenyewe limeniondoka;..” Danieli 2:5
Waganga na wachawi walitegemea labda watapewa chanzo cha ndoto hiyo ili wao waanzie hapo kutafsiri,lakini hali haikuwa hiyo.
Walitakiwa watafsiri ndoto ambayo haina chanzo chochote kile.Hii ilikuwa ni kazi kubwa kuliko maelezo,Hivyo hakuna aliyeweza kutafsiri ile ndoto,si wachawi,wala waganga,wala wabashiri,wala Wakaldayo.
Ndiposa wakamtafuta Danieli na wenzake ili wauwawe (Danieli 2:13) Maana walijua hata wakina Danieli na wenzake hawataweza kutoa majibu ya ile ndoto,sababu yeye aliyeiota kwanza haikumbiki lakini cha ajabu yeye aliyeota anahitaji majibu.
Haleluya…
Jambo moja la mdingi tunalojifunza siku ya leo ndilo hili;
*Hakuna hawezaye kufasiri ndoto asipoongozwa na Mungu.
Tunasoma;
  ” Ndipo Danieli akaenda nyumbani kwake,akawapasha habari kina Hanania,na Mishaeli,na Azaria wenzake;
ili waombe rehema kwa Mungu wa mbinguni kwa habari ya siri hiyo,ili kwamba Danieli na wenzake wasiangamizwe pamoja na wenye hekima wa Babeli.” Danieli 2:17-18
Jina la Bwana litukuzwe…
Nampenda Danieli tazama;
Danieli alipoitwa mbele ya mfalme hakuwa na haraka kusema,maana alijaa hekima za tofauti kabisa,naye Danieli alitambua jambo moja kwamba hata yeye mwenyewe hana uwezo wa kutafsiri ndoto ile,na akajua ya kwamba ni Mungu tu ndiye mwenye kutafsiri ndoto zote kwa msaada wa Roho Mtakatifu.
Danieli akapiga hesabu kubwa kisha akajua ahaa!
lazima amfuate Mungu aliye hai,Mungu wa utaratibu.
Ndiposa,Danieli akaenda kuwapasha habari rafiki zake.
Sasa unisikilize;
Upatapo jambo kubwa kama hilo yakupasa kuwaendea rafiki zako wa kiroho ambao mtaambatana kiroho.Wapo marafiki wasioambatana kiroho yaani marafiki wasiokuwa na roho moja na wewe.
Danieli aligundua hili,ndiposa akawaendea rafiki zake wenye roho moja. Ninaposema watu wenye roho moja nina maanisha watu walio tayari kubeba mzigo wako,pale unapokuwa na shida,basi shida hiyo nayo ni ya kwao,raha zako ni raha zao.
Kile utakachokiomba ndicho hicho hicho watakachokiomba.Watu wa namna hii ni watu wenye muambatano wa robo moja.
Haleluya…
Wakina Danieli wakaenda kumuuliza Bwana Mungu kwa habari ya kupewa majibu sahihi ya ndoto ya mfalme,naye Bwana akawajibu.
Oooh,Haleluya..
kile walichokishinda wanadamu,Mungu ameshinda.Mungu amefanya njia pasipo na njia.
Hivyo ifike wakati ambapo tusitumie akili zetu kupambanua ndoto,ni lazima.Pia tupatapo jambo lolote gumu,yatupasa kuwashilikisha wenzetu watu wa rohoni ili tuungane pamoja kuomba mbele za Mungu.
Wengi tunapata NDOTO katika nyakati hizi za mwisho,lakini swali la kujiuliza ;
Je tunazifanyia kazi ndoto tuotazo?
Ikiwa umeota ndoto,yakupasa kumuliza Mungu kwanza kabla ya mwanadamu yeyote yule.Hata baadaye ndipo waweza kumuuliza mtumishi wa Mungu.
Mungu huendelea kusema nasi kwa njia tofauti tofauti kabisa mfano aweza sema nasi kwa njia ya UNABII, MAONO na NDOTO (Mate do 2:17) kama tulivyojifunza.
MWISHO.
Najua utakuwa umebarikiwa sana kama wengine walionipigia simu jinsi walivyobarikiwa. Kumbuka jambo moja;
SAA YA WOKOVU NI SASA,
piga namba yangu hii,na Bwana atakuhudumia;
0655-111149.
@ Mtumishi Gasper Madumla.
UBARIKIWE.

MAONO NA NDOTO * sehemu ya saba *

picha g
Mtumishi Gasper Madumla.
Haleluya….
Nakusalimu nikikuambia;
Bwana Yesu asifiwe sana…
Leo tunaingia katika kipengele kipya kabisa kuhusu NDOTO.Maana katika siku sita zote tulikuwa tukijifunza kuhusu maono.
Wengi wametafsiri neno NDOTO kwa tafsiri tofauti tofauti,ingawa tafsiri nyingine si tafsiri sahihi. Leo tanajifunza tafsiri sahihi iliyo rahisi kabisa ya neno NDOTO.
Ndoto ni nini?maono 03
*Ndoto ni mtiririko wa picha zitembeazo katika akili ya mtu,pindi mtu huyo anapokuwa amelala.
Ndoto huja pale mtu anapokuwa amelala,na ndio maana huwezi kumkuta mtu ambaye ajalala,mtu atembeaye kisha akuambie ya kwamba alikuwa anaota ndoto wakati anatembea.
Hakika ukikutana na mtu kama huyo ni lazima utamshangaa !..
Na swali la kwanza utakalo muuliza mtu huyo ni hili;
“Je wakati unatembea ulikuwa umelala,hata uote?”
Na swali la namna hiyo ni swali la msingi kabisa,maana sote twajua kwamba; ili mtu aote inampasa alale.
Haleluya…
Groly to God….
vision 2Tofauti ya MAONO na NDOTO.usingizi 2
*Maono yanaweza kuonekana hata pasipo kulala,lakini NDOTO ni lazima muhusika alale ndipo aote
* Maono huusika na roho,wakati NDOTO huusika na akili.
Kumbuka;
Mtu anapolala roho yake i macho,roho ya mtu aliye hai ailali,hivyo mtu anaweza kupata maono akiwa hajalala au hata akiwa amelala(Kama tulivyojifunza siku sita za fundisho hili)
Lakini mtu hawezi kupata ndoto akiwa hajalala sababu ndoto husubiri kupumzika kwa akili.
*Maono huwa na maana na mafunuo ya msingi,NDOTO nyingi huwa hazina maana.
Ndiposa Mhubiri anasema;
 ‘‘ Kwa maana ndoto huja kwa sababu ya shughuli nyingi;…” Mhubiri 5:3
>Wengi huota kwa sababu ya miangaiko ya mchana kutwa,wakilala tu pale akili inapopumzika,nao huota. Ndoto za namna hii huwa hazina maana.
*Watu wengi huota ndoto,wachahe sana huona maono.
>Hapa sasa;
Ninajua hata wewe utakuwa umeshawahi kuota ndoto nyingi sana,hata nyingine huzikumbuki hivi sasa,lakini vipi kuhusu maono? UMESHAWAHI KUPATA MAONO YOYOTE?
Leo hii wakitokea watu wawili kisha mmoja aanze kusema hivi;
“…Jana nilikutana na Mungu,akanionesha mambo makubwa kisha Mungu akaniambia…
Huyu mtu wa kwanza,hawezi kuaminika kiurahisi kwa ushuhuda wake wa kuonana na nguvu za Mungu maana watu watamshangaa ! wakihoji kwamba inawezekanaje akutane na Mungu?
Haya;
Mtu wa pili naye aje na kusema hivi;
“…Jana nilikutana na shetani na mapepo yake….”
Watu wa leo watamuamini zaidi,na kumsikiliza huyu wa pili kwa sababu eti amekutana na shetani na mapepo yake.Ushuhuda wa mtu wa pili umepewa nafasi zaidi ya ushuhuda wa mtu wa kwanza aliyeshuhudia amekutana na Mungu/Nguvu za Mungu katika maono.
Bwana Yesu asifiwe sana…
Mimi siwashangai sana watu wa namna hiyo, wale wenye kukataa kumuamini mtu yule wa kwanza aliyesema ameonana na Mungu sababu kupata MAONO juu ya nguvu za Mungu sio rahisi hata kidogo,tofauti na kuonana na shetani na mapepo yake.
Ndio maana ninakuambia MAONO hupatikana kwa nadra sana,MAONO makubwa ni kwa wale watu wa rohoni,Bali NDOTO ni kwa watu wote.
Haleluya…
Ndoto ni njia mojawapo ya mawasiliano ya ki-Mungu au hata ya kipepo pia.
Nasema ni mawasiliano ya ki-Mungu kwa maana tumeona Mungu akisema na watu wake wengi katika ndoto,akiwaonya,akiwapa maelekezo,au akisema nao juu ya mambo yajayo.
Tazama hapa;
 ‘‘ Na hao walipokwisha kwenda zao,tazama,malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto akasema,Ondoka,umchukue mtoto na mama yake,ukimbilie Misri,ukae huko hata nikuambie;kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize.” Mathayo 2:13.
Bwana Mungu anamfikishia taharifa Yusufu kwa njia ya malaika,akimueleza mabaya yanayotarajiwa kufanywa na Herode.
Ndoto ikawa kama chombo cha kukamilisha taharifa ya Mungu kwa Yusufu.Vivyo hivyo Mungu anaeweza kusema nawe kwa njia ya malaika juu ya mambo ya hatari ndani ya maisha yako.
Biblia inaweka wazi ya kwamba Bwana Mungu hujifunua katika maono,lakini husema nasi katika ndoto;
”  Kisha akawaambia,
Sikilizeni basi maneno yangu;
Akiwapo nabii kati yenu,
Mimi,Bwana,nitajifunua kwake katika maono,
Nitasema naye katika ndoto.” Hesabu 12:6
Haleluya…
Katika nyakati hizi za mwisho,Bwana bado husema nasi katika ndoto,akitufunulia mambo yajayo….
ITAENDELEA…
UBARIKIWE.

MAONO NA NDOTO * sehemu ya sita *

vision
Na Mtumishi wa Mungu Gasper Madumla.
Bwana Yesu asifiwe…
Haleluya…
Msingi wa fundisho letu ndio huu hapa;
Tunasoma;
 ” Itakuwa siku za mwisho,asema Mungu,nitawamwagia watu wote Roho yangu,na wana wenu na binti zenu watatabiri;na vijana wenu wataona maono;na wazee wenu wataota ndoto.” Matendo 2:17
Karibu siku ya leo tunapoendelea kujifunza fundisho hili lenye msingi wa maisha yako wewe mkristo, hata wewe ambaye yamkini si mkristo,maana kupitia fundisho hili, yapo mambo yenye uwezo mkubwa wa kukutoa kiroho hapo ulipo na kukupeleka kiwango kingine cha kiroho kadri tunapoendelea kutafakari juu ya MAONO.
Kumbuka nilikupa maana nyingi zaidi kuhusu neno MAONO,ili kupanua uelewa wako.
Haleluya…
Kanisa bila maono hupotea,alikadhalika mkristo bila maono hupotea.Ili tuweze kukua vizuri kiroho ni lazima tujue ni wapi tunaelekea,ili kujua ni wapi unaelekea ni lazima uwe na MAONO.
Kila mmoja wetu amewekewa kusudi na dhumuni fulani katika maisha yake.Kusudi hilo ndio MAONO,ambayo hayo maono ndio sababu ya wewe kuishi hapa duniani.
Leo hii nyumbani mwa BWANA,watu wengi wanaishi pasipo kujua MAONO yao waliyowekewa tayari kwa ajili ya kazi ya Bwana.Ndio maana kanisa au huduma inakuwa ngumu sana.Ninampenda MUSA alipotokewa na malaika wa BWANA,pale alipotumwa akaifanye kazi ya Bwana Mungu kwa kuwaokoa waisraeli kutoka mikononi mwa Farao,Musa anaanza kwa kumuuliza Mungu kusudi aliloitiwa;
Musa akamwambia Mungu, Tazama, nitakapofika kwa wana wa Israeli, na kuwaambia, Mungu wa baba zenu amenituma kwenu; nao wakaniuliza, Jina lake n’nani? Niwaambie nini? ” Kutoka 3:13
Alichokitafuta Musa hapo ni kupata maelezo sahihi kwa ile kazi ya Bwana Mungu anayomtuma ndani ya yale MAONO.Musa hakuifanya kazi hiyo ya Bwana Mungu kwa akili zake,
bali alihitaji sana aoneshwe na kupewa maelekezo sahihi. Ndiposa Mungu anamjibu Musa ya kwamba Yeye Mungu jina lake nani. Hapo sasa Musa akawa na mwanzo mzuri wa kuianza kazi ya Bwana Mungu.
Leo hali imebadilika kabisa,mara nyingi mtumishi wa Mungu huanza kazi ya Mungu then,baadaye;katika kazi hiyo aliyokuwa ameianza yeye mwenyewe ndio utamkuta akiomba msaada wa Mungu,Swali la kujiuliza;
Kwa nini asianze kumuuliza Mungu kwanza ndipo aifanye?
Haleluya…
Mkutano Tanga 02
Watu wengi hupenda kufanya kazi ya Mungu pasipo kuelezwa kwa usahihi wa kazi hiyo na Mungu mwenyewe.
Usifanye kazi ya Bwana Mungu ikiwa hukupewa maelekezo sahihi na Mungu mwenyewe.
• Maelekezo ya Mungu ni MAONO katika utumishi wako.
Maana wapo watu wajiitao ni wachungaji,hali hawakupewa maono ya kuwa wachungaji,Tena
Wapo watu wajiitao ni mitume,hali hawakupewa maono ya kuwa mitume.N.K
Mwache Bwana mwenyewe ajifunue katika MAONO juu ya kile alichokiitia,ili utakapoanza kufanya hilo kusudi la Mungu mwenyewe basi Yeye Mungu mwenyewe atajipigania na kujitetea katika kusudi lake lililo ndani yako maana si wewe ufanyaye bali ni Mungu ndie afanyaye ndani yako.
Shida kubwa tuliyonayo hivi sasa ni kwamba;
Watu wengi hawajui MAONO yao.Wengine hutembea katika utumishi kwa kubahatisha,sababu ya kukosekana kwa ufumbuzi wa MAONO.Hii ni hatari !
Biblia imeweka wazi ya kwamba nyakati za mwisho,watu wataono maono baada ya ujazo wa Roho mtakatifu(Matendo 2:17).
Ikiwa maono yamekosekana,basi ujue mahali ulipo hakuna udhihilisdho wa nguvu za Roho mtakatifu,sababu MAONO hushushwa na nguvu za Roho mtakatifu….
ITAENDELEA….
UBARIKIWE.

MAONO NA NDOTO * sehemu ya tano *

vision
Na Mtumishi wa Mungu Gasper Madumla.
Bwana Yesu asifiwe…
Haleluya…
Tunasoma;
Itakuwa siku za mwisho,asema Mungu,nitawamwagia watu wote Roho yangu,na wana wenu na binti zenu watatabiri;na vijana wenu wataona maono;na wazee wenu wataota ndoto.” Matendo 2:17
Haleluya….
Jina la Bwana libarikiwe….
Andiko tulilolisoma hapo juu,ndilo andiko letu la kusimamia fundisho letu zuri. Kupitia andiko hilo,tulijifunza kuhusu KUTABIRI kwa mujibu wa maandiko matakatifu na tukaangalia mifano ya watu waliopata kutabiri,kisha tukajifunza kuhusu MAONO.
Leo ni siku ya tano tukijifunza juu ya MAONO.
Tulijifunza kuhusu maono kama ishara ya picha halisi juu ya tukio lijalo lenye kuonekana katika ulimwengu wa kiroho,tukaenda kiundani sana kuangalia na aina za maono,pamoja na mifano yake( Fuatilia sehemu zilizopita)
Leo tunajifunza kuhusu maono kwa mtizamo mwingine.
Kumbuka;
Nilikuwaambia kwamba,kila mwanadamu chini ya jua ameumbwa kwa maana na kusudi maalumu la Mungu mwenyewe. Nikakuambia ya kwamba,hakuna mwanadamu aliyeumbwa kwa bahati mbaya.
Haijalishi wewe ni mkristo au si mkristo lakini ujue ya kwamba hukuumbwa kwa bahati mbaya.Mungu anakuhitaji akuokoe kwa wokovu ulio mkuu kupitia jina la Yesu Kristo wa Nazareti.
Hivyo basi kama hukuumbwa kwa bahati mbaya ,basi uliumbwa kwa bahati nzuri ya kuyafanya mapenzi ya Baba wa mbinguni.
Ikiwa ni hivyo basi,
Tafsiri nyingine ya MAONO ni ipi?
vision 2
MAONO ni ufumbuzi wa kusudi la Mungu na mpango wa Mungu ndani ya maisha yako.
Haleluya…
Nasema MAONO ni ufumbuzi wa mpango na malengo ya Mungu ndani ya maisha yako,
Au,
Kwa lugha nyingine mmoja anaweza sema MAONO ni Kusudi la ki-Mungu uliloumbiwa. Yaani ni kwa nini uliumbwa mwanadamu,ile sababu iliyokufanya uumbwe hivyo ulivyo wewe mwanadamu,sababu hiyo ndio inaitwa MAONO.
Bwana Yesu asifiwe…
Kama ningekuwa nakufundisha kwa lugha ya kiingereza ningekuambia;
VISION is the discovery of divine purpose and plan in your life.
Dhumuni kubwa la kuumbwa mwanadamu ni kumuakilisha BWANA MUNGU hapa duniani. Katika kumuakilisha BWANA MUNGU hapa chini ya jua,ndio namna ya kuyafanya mapenzi yake katika DHUMUNI na LENGO fulani la Mungu mwenyewe.
Hilo dhumuni na lengo fulani lililofichika ndilo huitwa MAONO au VISION.
Mfano;
BWANA MUNGU anataburisha dhumuni la kumuumba Yeremia akisema;
Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua,na kabla hujatoka tumboni,nalikutakasa;nimekuweka kuwa nabii wa mataifa. ” Yeremia 1:5
Bwana Mungu anaelezea dhumuni na lengo kamili la kuumbwa kwa Yeremia,kwamba Yeremia aliumbwa ili awe nabii wa mataifa.
Lile dhumuni la kutengwa kwa Yeremia,awe nabii ndio MAONO.
Maono hayo yalikuwa katika hali ya kufichika,kwamba hakuna mwanadamu mwenye kuyajua hayo,isipokuwa ni Mungu pekee ndiye aliyekuwa akijua MAONO ya kuumbwa kwa Yeremia.
Haleluya…
Hata wewe,kabla hujaumbwa katika tumbo la mama yako,BWANA alikujua,alikutakasa,na alikutenga kuwa mtu fulani katika kazi yake Mungu hapa chini ya jua. Hiyo ” kazi fulani ya Mungu hapa chini ya jua uliyoumbiwa…” Ndio hujulikana kama MAONO.
Mungu alikujua kabla hujaumbwa tumboni,na pia alikutakasa,na zaidi ya yote ulitengwa kwa kazi ya Bwana.
Ngoja nikupe mfano mwingine hapo;
BWANA MUNGU anatambulisha pia dhumuni la kumuumba Yohana mbatizaji.
Tunasoma;
 ” Kwa sababu atakuwa mkuu mbele za Bwana;hatakunywa divai wala kileo;naye atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye. Na wengi katika Waisraeli atawarejeza kwa Bwana Mungu wao.’‘ Luka 1: 15-16
Bwana Mungu anazidi kutuelezea dhumuni na lengo la kumuumba Yohana mbatizaji. Anasema Yohona alikusudiwa kuwalejeza wengi katika Waisraeli,kuwalejeza kwa Bwana Mungu wao kwa njia ya toba ya ubatizo wa maji.Yohana ndiye aliyepewa kusudi la kutengeneza njia ya Bwana Yesu.
Haleluya..
Maono ni ufumbuzi wa kazi ya ki-Mungu ndani ya maisha ya mtu.
Ngoja niendelee kukupa mifano zaidi kuhusu maono katika mtazamo huu wa pili.
Bwana Mungu anazidi kutueleza kusudi la uumbaji kwa watu wake. Na hapa anatueleza kusudi na lengo maalumu la kumuumba Sauli,
Tunasoma;
Kesho wakati kama huu,nitakuletea mtu kutoka nchi ya Benyamini,nawe mtie mafuta ili awe mkuu juu ya watu wangu Israeli,naye atawaokoa watu wangu na mikono ya Wafilisti;maana nimewaangalia watu wangu,kwa sababu kilio chao kimenifikilia.”1 Samweli 9:16.
Maono ya kuumbwa kwa Sauli,yalikuwa ni kuwaokoa wana wa Israeli kutoka katika mikono ya Wafilisti,maana kilio chao kilimfikilia Bwana Mungu.
Sauli hakuwa na maono ya ubatizaji,Bali maono ya kuwaokoa Waisraeli kutoka kwa Wafilisti.
Alikadhalika tunaona dhumuni na kusudi la kuumbwa kwa mtume Paulo,Paulo hakuumbwa awe mbashiri wa ndoto,Bali aliumbwa ili awe mtume wa mataifa.Kuwa mtume wa mataifa ni maono ambayo yalikuwa ndani ya Paulo hata kama hapo awali alikuwa ni muuaji,lakini Bwana Mungu alikwisha mtenga awe mtume wa mataifa. (Wagalatia 1:15-16)
Haleluya,…..
Glory to God…
Pia tunaona Maono ya ujio wa Bwana Yesu Kristo chini ya mbingu.Maono ya ujio wa Bwana Yesu Kristo yalikuwa ni kuokoa kile kilichopotea.Kuwaokoa watu na dhambi zao. Pia Yesu Kristo amebeba kusudi la kurejesha ushirika wa Roho mtakatifu,ushirika ule uliopotea pale katika bustani ya Edeni.
ITAENDELEA…
UBARIKIWE.

MAONO NA NDOTO * sehemu ya nne *

maono 01
Maono hupatikanika mara chache ukilinganisha na ndoto.
Bwana Yesu apewe sifa…
Nakusalimu mpendwa katika jina la Bwana,nikisema;
Haleluya…
Leo ni siku ya nne ya fundisho hili mahali hapa.Wengi waliokuwa wakifuatilia fundisho hili kwa njia ya mtandao wanasema;
wamebarikiwa sana na wamepokea mafunuo mengi kupitia fundisho hili.
Kumbuka;
Tulikuwa tukijifunza namna ya maono yanavyoweza kukamilishwa.Tukaangalia njia mbili ambazo MAONO hukamilika,njia hizo ni njia ambazo maono yanaweza kupitia,nazo ni;
(a)Maono kwa njia ya macho ya wazi wazi.
(b)Maono kwa njia ya usingizi./Kuzimia kwa roho.
maono
Mtu huweza kupata maono kwa macho ya wazi wazi pasipo kulala.
(Fuatilia sehemu zilizopita,ili uelewe vizuri mahali tulipotoka)
Haleluya…
Sasa tunaendelea;
Biblia inasema;
Nalikuwa katika Roho,siku ya Bwana;nikasikia sauti kuu nyuma yangu,kama sauti ya baragumu”  Yohana 1:10
Katika andiko hilo,tunaposoma ya kwamba “nikasikia…..sauti kama ya baragumu”
lile neno ” nikasikia…
lina maanisha kwamba;
masikio ya rohoni ndio yalisikia ile sauti iliyo kama ya baragumu kwa sababu Yohana alikuwa katika roho.
Kwa lugha nyingine Yohana hakusikia ile sauti kwa masikio yake ya damu na nyama,Bali alisikia kwa masikio ya rohoni. Hivyo basi ikiwa Yohana alipata kusikia sauti pindi alipokuwa rohoni,basi;inaonesha yapo masikio ya rohoni yenye kusikia sauti ya BWANA MUNGU.
Yohana ilipokuwa akiyapata maono hayo alikuwa kama mtu aliyekufa (Yohana 1:17). Ndio maana maono haya hujulikana kama maono kwa njia ya usingizi.
Haleluya…
Sasa unisikilize tena;
Tumeaona watu waliopata maono makubwa kama akina Yohana,Musa,akina Ezekieli,pamoja na Samueli,pamoja na Petro,pamoja na Kornelio,N.K ;
hao wote wakiwa wamepata maono kwa njia ya usingizi/kuzimia kwa roho au kwa njia ya macho ya wazi wazi kama tulivyojifunza hapo awali.
Watu hao waliopata maono,walikuwa ni watu wa rohoni. Watu wenye kubeba kusudi la Mungu. Nasi leo hii tukitaka kuwa na MAONO makubwa kama hayo ni lazima tuwe watu wa rohoni kweli kweli.
Mungu huzungumza nasi kwa njia nyingi,na kwa njia tofauti tofauti; miongoni mwa njia hizo ni njia ya MAONO.Shida moja tuliyokuwa nayo leo ni kukosa MAONO. Ikiwa tunakosa maono,
Basi ipo shida ndani yetu.
Si kana kwamba Mungu hasemi nasi siku za leo,Au
Si kana kwamba Mungu hakuachilia nguvu ya maono kwa watu wake,Bali maono yamekwisha achiliwa (Matendo 1:17) lakini shida tuliyonayo sisi ni MIKAO yetu tuliyokaa ndani ya maisha ya ukristo,mikao yetu hayampendezi BWANA MUNGU.
Sasa,
Ikiwa kama tunataka kuwa na maono makubwa kama waliyoyaona watu wa Mungu wa kipindi kile,basi ni lazima tubadili mikao yetu mbele za BWANA MUNGU.Mikao yetu ya kubadili ni kukubali kutoka rohoni kuishi maisha ya utakatifu na kuzichukia dhambi zote.
Sikia;
Watumishi wa Mungu wa kipindi kile walikuwa hawafanyi jambo lolote pasipo kuoneshwa katika MAONO. Watumishi wa Mungu walihitaji kupewa ufafanuzi na maelekezo juu ya kazi waliyoitiwa,mfano;
Musa alipopata maono ( Kutoka 3:1-3) pale alipotumwa aende kwa Farao.
Musa alihitaji kujua maelezo sahihi,namna ya kuanza na kumaliza kazi aliyopewa na BWANA MUNGU,ndio maana Mungu anaanza kumuelekeza ya kwamba yeye ni Mungu wa namna gani aliyemtokea,anaanza kumwambia ya kwambaYeye Mungu anaitwa nani/jina lake Mungu ni lipi,
kisha anamtuma.
Hayo yalikuwa maelezo muhimu sana kwa Musa.Pia watu wa Mungu walikuwa wakihitaji kuona MAONO juu ya kazi yoyote ile waliyopewa na Bwana Mungu.
Walikuwa hawaendi kuifanya kazi ya Mungu kwa shauli lao.
Leo,watumishi wamekosa MAONO,Bwana Mungu hakujifunua kwao,kwa sababu ya maisha yao ya dhambi,na wengi huenda kwa kutumia akili zao,na ndio maana huduma inakuwa ngumu sana sababu MAONO hakuna.
Bwana Yesu asifiwe…
Ni maombi yangu,ya kwamba Mungu akaturehemu sisi watumishi wa Mungu wa Tanzania ili tuweze kupata MAONO juu ya huduma tuzifanyazo.
Haleluya…
Nasema;
Maono tuliyojifunza,ni maono kama ishara ya picha. Tafsiri hiyo ya maono kama ishara ya picha ni moja ya tafsiri kubwa sana ambayo waandishi hata walimu wengi hawaielezei kiundani kama sisi tulivyojifunza takribani siku nne mfululizo.
Sasa ;
Imefika wakati wa kukupa tafsiri nyingine ya Maono. Ninaomba uwe makini kabisa kunifuta,ili uelewe vizuri.
Naanza hivi;
Kila mwanadamu aliyeumbwa,aliumbwa kwa maana na kusudi kamili la BWANA MUNGU mwenyewe. Mwanadamu hakuumbwa kwa hasara. Ndio maana Mungu alipomuumba mwanadamu na vitu vingine akaona ya kuwa ni vjema. (Mwanzo 1:31)
Na ikumbukwe ya kwamba, Mungu alihakikisha anamuwekea mwanadamu kila kitu tayari ili mwanadamu aje afanye kazi ya kuvitawala vile vilivyoumbwa…
ITAENDELEA….
@Mtumishi Gasper Madumla.
Nakuomba sana usikose kabisa fundisho lijalo. Maana lipo neno litakalo kusaidia sana tunapoendelea kujifunza juu ya MAONO na NDOTO.Hapa tulipoishia,bado sijakuelezea kiundani juu ya tafsiri ya hii ya pili ya neno MAONO kwa mujibu wa biblia. Yashike sana hayo,ili tukiendelea tuwe pamoja.
• Kwa huduma ya maombi na maombezi,piga namba hii;
0655-111149.
UBARIKIWE.

MAONO NA NDOTO * sehemu ya tatu *

maono 4
Fuata ndoto zako.
Bwana Yesu asifiwe…
Jina lake BWANA MUNGU na lihimidiwe na kila mwenye pumzi na aseme;
AMINA…
Karibu katika sehemu ya tatu ya fundisho hili zuri sana.
Leo tunaendelea tena;
Kumbuka;
Nazungumzia MAONO
Fundisho lililopita tulijifunza kwamba maono yanaweza kukamilishwa kupitia njia mbili. Au kwa lugha nyingine ni kwamba ;
Mtu anaweza kupata MAONO kupitia njia kuu mbili nazo ni;
* Maono kwa njia ya macho ya wazi wazi.
*Maono kwa njia ya usingizi/kuzimia kwa roho.
fundisho lilopita tuliangalia kidogo katika sehemu ya maono kwa njia ya macho ya wazi wazi ikiwa ni njia mojawapo ya kukamilisha maono.Leo tunamuangalia mtu mwingine aliyepata maono kwa njia isiyo ya usingizi./Maono kwa njia ya macho ya wazi wazi.
Mfano mmojawapo mwingine wa mtu aliyepata maono kwa njia ya macho ya wazi wazi ni ; Musa.
Tunasoma;
Malaika wa BWANA akamtokea,katika mwali wa moto uliotoka katikati ya kijiti;akatazama,na kumbe !kile kijiti kiliwaka moto,nacho kijiti hakikuteketea. Musa akasema, Nitageuka sasa,niyaone MAONO haya makubwa,na sababu kijiti hiki hakiteketei. ” Kutoka 3:2-3
Musa alipata maono haya akiwa yupo macho. Kwa lugha nyingine Musa hakuwa amelala,Bali alikuwa U macho,ndiposa malaika wa BWANA akamtokea Musa katika mwali wa moto katikati ya kijiti kiwakacho pasipo kuteketea.
BWANA MUNGU alikuwa akimuandaa Musa kukaa katika mkao ambao NENO lake Mungu lipate nafasi ndani ya Musa.
Ndiposa,
Bwana akamfanyia Musa kama kituko vile cha kuwasha moto katika kijiti kisichoteketea. Kituko hiki kilimuandaa Musa kusikia sauti ya Bwana maana Musa alitekewa na mazingira,na BWANA akazungumza na Musa.
Mungu pia anaweza kuzungumza na wewe kwa njia hii ya maono kwa macho ya wazi wazi,akitumia kituko fulani ili aukamate moyo wako,na neno lake BWANA lipate nafasi ndani yako,kama vile alivyojifunua kwa Musa.
Hivyo ;
hiyo ni njia moja ya maono,ambapo mtu aliye rohoni akipata maono kwa njia ya macho ya wazi wazi.
maono 5
Watu wengi huota wakiwa wanapaa,nyakati za usiku

02.MAONO KWA NJIA YA USINGIZI.
Hii ni njia ambayo mtu hupata maono akiwa amelala.
Njia hii ni njia ya pili ambayo maono hupitia kwa mlengwa akiwa amelala. Maono yanayopitia njia hii ya usingizi sio ndoto,Bali ni maono.Ipo tofauti kati ya MAONO na NDOTO,lakini hapa nazungumzia MAONO na wala sio ndoto.
Tunasoma;
Kwa hiyo Eli akamwambia Samweli,Enenda,kalale;itakuwa,akikuita,utasema,Nena,BWANA;kwa kuwa mtumishi wako anasikia.Basi Samweli akaenda akalala mahali pake.BWANA akaja,akasimama,akaita vile vile kama kwanza,Samweli ! Samweli ! Ndipo Samweli akasema,Nena BWANA,kwa kuwa mtumishi wako anasikia.”  1 Samweli 3:9-10
Haleluya…
Biblia inasema BWANA alimuita Samweli mara tatu,na kila Samweli alipoitwa,alimkimbilia kuhani wake Eli akidhani ya kuwa Eli amemwita,kumbe alikuwa akiitwa na BWANA.
Eli naye hakutambua sauti ya BWANA kwa mara hizo zote tatu;BWANA alipomuita Samweli,kwa sababu siku zile NENO LA BWANA lilikuwa adimu na wala hapakuwa na mafunuo dhahili ( 1 Samweli 3:1).
Hivyo hata kuhani Eli hakuwa na mafunuo dhahili ndio maana hakuweza kuitambua sauti ya BWANA kwa urahisi.
Haleluya…
BWANA alimuhitaji Samweli aende kulala ndipo BWANA ajifunue kwake,kama tulivyosoma hapo juu,Samweli anaambiwa aende kulala tena ili BWANA apate nafasi ya kujifunua kwake.
BWANA hakujifunua kwa Samweli katika ndoto,Bali BWANA alijifunua katika MAONO.
Samweli hakuwa akiota ndoto,Bali alienda kulala ndipo BWANA akajifunua;maana tunasoma;
“…Basi Samweli akaenda AKALALA mahali pake.BWANA akaja,AKASIMAMA,akaita…” (1 Samweli 3:9-10)
Tunaposoma ;
“..BWANA akaja, akasimama…”
maana yake BWANA alijifunua katika maono. Lakini alijifunua pale Samweli alipokuwa amelala.
Swali moja ambalo waweza kujiuliza kama vile mimi nilivyojiuliza,ni kwamba;
*Je kwa nini BWANA hakujifunua kwa Samweli pale alipomuita Samweli kwa mara ya kwanza?
Au,
* Kwa nini BWANA alimuhitaji Samweli amjibu kwamba ” Nena, BWANA ;kwa kuwa mtumishi wako anasikia”ndipo BWANA aanze kujifunua na kuanza kunena na Samweli,na asinene naye tu hivyo hivyo?
Umeelewa hapo?
Haleluya…
Ok,
Ndiposa nikapata JIBU,kwamba;
BWANA alihitaji Samweli afungue moyo wake ili neno lake BWANA likapate nafasi,maana kuanzia hapo Biblia inasema ;
Samweli hakuliacha neno BWANA lipotee/lianguke chini” ( 1 Samweli 3:19)
Siku ya leo,BWANA huzungumza nasi kwa maono pia,lakini BWANA anatuhitaji tufungue mioyo yetu kwanza na kuwa tayari kusema
Nena nasi,kwa kuwa sisi watumishi wako tunakusikia”
Tukifaulu kuifungua mioyo yetu,neno la BWANA litapata nafasi ndani yetu.
Alikadhalika kupitia njia hii ya maono kwa njia ya usingizi,Tunamuona Yohana (Yohana mtume wa Yesu) alipokuwa katika kisiwa cha Patmo siku ya Bwana. Biblia inatuambia;
Nalikuwa katika Roho,siku ya Bwana ; nikasikia sauti kuu nyuma yangu,kama sauti ya baragumu,” Ufunuo 1:10
Biblia inaposema “….Nalikuwa katika Roho…” ina maana kuwa Yohana hakuwa na ufahamu wa kawaida,yaani akili za Yohana zilikuwa hazina matunda,Bali roho yake ndio ilikuwa hai,halisi,roho yake ilikuwa ‘‘ active’‘/roho yake Yohana ilikuwa ikizungumza na BWANA.
Sikia;
Mtu akiwa Rohoni,akili hufa.
Na ndio maana njia hii ya MAONO hujulikana kuwa ni maono kwa njia ya usingizi,maana katika usingizi ni nusu ya kufa,lakini roho huwa halisi,sababu roho hailali,kinacholala ni akili tu.
Haleluya…
Tazama hapa;
Nami nilipomwona,nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa…” Ufunuo 1:17
Maono haya aliyoyaona Yohana yalikuwa makubwa sana. Yohana alikuwa kama mtu aliyekufa,kwa sababu alikuwa kama amelala,Akili zake hazikuwa na kazi tena,Bali roho yake ilikuwa hai.
*Kumbuka nazungumzia MAONO yaonekanayo kwa njia isiyo ya macho ya wazi wazi./Njia ya usingizi.
Haleluya…
Yohana hakuwa anaota,Bali alikuwa akipata MAONO kwa njia ya roho yake,maana pale tusomapo kwamba Yohana alikuwa kama mtu mfu,maana yake akili,utashi,fahamu zake hazikuwa hai Bali roho tu ndio ilipata nafasi ya kuona…
ITAENDELEA…
@ Mtumishi Gasper Madumla.
UBARIKIWE.

MAONO NA NDOTO * sehemu ya pili *

Mtumishi akifundisha
Mtumishi Gasper Madumla.
Bwana Yesu asifiwe…
 “Itakuwa siku za mwisho,asema Mungu,nitawamwagia watu wote Roho yangu,na wana wenu na binti zenu watatabiri ; na vijana wenu wataota maono ; na wazee wenu wataota ndoto” Matendo 2:17
 Andiko hilo hapo juu ndilo andiko letu la kusimamia fundisho letu la MAONO na NDOTO.
 Biblia inaweka wazi kabisa ya kwamba nyakati za mwisho Bwana Mungu atamwaga Roho yake kwa watu wote,na mara tu ya Roho wa Mungu kuwashukia watu,Biblia inatuambia ya kwamba wana na binti watatabiri.
Nasi tulijifunza kwa undani kidogo juu ya KUTABIRI na tukaangalia watu waliopata kutabiri katika maandiko matakatifu.
 Ila jambo moja la msingi ni kwamba;
 Wale wote waliotabiri,walitabiri baada ya kushukiwa na nguvu za Roho mtakatifu.
 Hivyo suala la kutabiri husimamiwa na kuongozwa na nguvu za Roho mtakatifu,kama vile biblia isemavyo hapo juu (Matendo 2:17)
Kwa lugha nyingine;
 ni kwamba, hakuna anayetabiri jambo au mambo ya ki-Mungu kwa kujiongoza yeye mwenyewe.
Haleluya…
naamini tupo pamoja hadi sasa.
Katika andiko letu la Matendo 2:17.Tunaona mambo matatu yakizungumziwa,kwamba yatatoke mara baada ya mwagiko wa Roho wa Mungu.
 tukio la kwanza ni KUTABIRI (kama tulivyojifunza katika sehemu ya kwanza)
Tukio la pili na la tatu baada ya Roho wa Mungu kumwagwa kwa watu ni;
 *MAONO na
 *NDOTO
Haleluyaa…
01.MAONO
Zipo tafsiri nyingi zinazoelezea maana ya neno maono. Na inawezekana hata wewe unatafsiri yako kuhusu maono.
 Lakini nakushauri uchukue tafsiri hii nikupayo siku ya leo,kwa maana itaongeza ufahamu wako kwa namna ya tofauti kabisa.
Nami ninakupa tafsiri zaidi ya mbili ili yamkini kama ulikuwa ukielewa moja tu,basi hizo nyingine ziwe faida kwako.
Maono ni nini?
 *Kwa mujibu wa maandiko matakatifu;
 Maono ni ishara za picha halisi zionekanazo katika ulimwengu wa roho zenye kutambulisha tukio lijalo katika ulimwengu wa kimwili.
Nisemapo kwamba ” ishara za picha halisi ” ninazungumzia ,picha ambazo sio za maigizo au sio picha za bandia,Bali ni picha halisi. Mfano,mtu anaweza kuona picha yako katika ulimwengu wa roho jinsi ulivyo hivyo hivyo ndani ya tukio fulani ambalo tukio hilo baada kukamilika kiroho,hudhihilika katika ulimwengu wa kimwili.
Na ukumbuke kwamba ;
 Jambo lolote ulionalo sasa limetokea ujue limekwisha tokea katika ulimwengu wa roho.
 Hivyo,
 matukio yote yanayotokea hivi sasa chini ya jua,mfano matukio ya mauaji ya walemavu,na mauaji mbali mbali,matukio kama vile maandamano N.K
Matukio hayo yote yalikuwa katika mfumo wa picha katika ulimwengu wa roho,na baada tu ya picha hizo kukamilishwa katika ulimwengu wa kiroho,sasa yanapewa ruhusa kudhililika katika macho ya damu na nyama
Maandiko yanatuambia;
”  …hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri.” Waebrania 11:3
Haleluya…
Nasema; Haleluyaa…
*Maono ni kielelezo kwa njia ya picha ndani ya roho ya mwonaji,kielelezo chenye kueleza tukio lililopita au hata lijalo.
 maono yanaweza kuwa ni picha za matukio yaliyopita YENYE HALI YA KUENDELEA.
Mfano wa maono katika matukio yaliyopita yenye hali ya kuendelea.
 Mtizame mtume Paulo mtu ambaye hapo awali alikuwa ni mtesaji wa watu wenye imani kwa Kristo Yesu.
 Paulo hakuwa mmoja wa mitume kumi na wawili waliochaguliwa na Bwana,lakini sasa tazama baada ya kufanywa awe mtumwa wa Kristo Yesu,mtume kwa watu wote. Ana hubiri habari za Bwana Yesu kana kwamba ni mtu aliyekuwa naye siku zote za Bwana Yesu.
Swali la kujiuliza,
 Alipataje kunena habari za Bwana Yesu kwa ufasaha, na kuna kipindi anahubiri injili kana kwamba yupo na Yesu ana kwa ana?
JIBU;
 Alikuwa akiwezeshwa na Roho mtakatifu kuona MAONO juu ya maisha ya Bwana Yesu Kristo,ambayo maisha ya Bwana yalikuwa yamepita lakini yalikuwa halisi yakiendelea ndani yake.
Nimekuambia pia maono yanaweza kuwa ishara za matukio yaonekanayo rohoni,matukio yanayotambulisha matukio yajayo katika ulimwengu wa kimwili.
Swali moja la ziada ambalo waweza kujiuliza ;
 Je ni kwa njia ipi mtu aweza kuona maono?
JIBU.
 Zipo aina kuu mbili za njia ambazo maono hupitia,nazo ni
 01.Maono kwa njia ya macho ya wazi wazi.
 02.Maono kwa njia ya usingizi-kuzimia kwa roho.

(A)MAONO KWA NJIA YA MACHO YA WAZI WAZI.
 Tunasoma;
Palikuwa na mtu Kaisaria,jina lake Kornelio,akida wa kikosi kilichoitwa kiitalia,mtu mtauwa,mchaji wa Mungu,yeye na nyumba yake yote,naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi,na kumwomba Mungu daima.
Akaona katika maono WAZI WAZI kama saa tisa ya mchana malaika wa Mungu,akimjia na kumwambia,Kornelio!”Matendo 10:1-3
Haleluya…
Biblia inatuambia kwamba;
 Kornelio alipata MAONO ya wazi wazi,ikimaanisha kwamba Kornelio hakuwa amelala,Bali alikuwa macho kama hivi wewe ulivyo macho muda huu.
 Ndiposa;
 Bwana akamtokea katika njia ya maono kwa macho ya wazi wazi kwa msaada wa Roho mtakatifu.
Biblia inatuambia;
Bwana hujifunua katika maono,pia husema katika ndoto” Hesabu 12:6
Bwana alijifunua kwa Kornelio katika maono. Kwa lugha nyingine ni kwamba;
 Bwana hajifunui katika ndoto,Bali katika ndoto Bwana husema,
 Lakini kwa njia ya MAONO tu,ndipo Bwana hujifunua….
Kumbuka;
 Nazungumzia MAONO.
ITAENDELEA…
Fundisho lijalo nitakupa mfano wa pili wa maono kwa njia ya macho ya wazi wazi,kisha tutaingia kwa undani kuangalia njia ya pili ya maono kwa njia ya USINGIZI.
Maono kwa njia ya usingizi wala sio ndoto Bali ni MAONO.
 *Je ungependa kujua zaidi na kujua tofauti kati ya ndoto na maono kwa njia ya usingizi?
BASI,USIKOSE FUNDISHO LIJALO!.
Kwa huduma ya maombi na maombezi,piga;
 0655-111149.
 UBARIKIWE.

MAONO NA NDOTO.*sehemu ya kwanza *

Mtumishi akifundisha
Mtumishi Gasper Madumla.
Bwana Yesu asifiwe…
Haleluya…
Nasema,
 Haleluya…
Ninakukaribisha katika fundisho zuri lenye kichwa cha habari kisemacho,MAONO na NDOTO.
 Kati ya mambo ambayo watu hutafuta kujua ufafanuzi na maana halisi kwa mambo yajayo au yaliyopita ni MAONO na NDOTO.
 Hakuna mwanadamu chini ya jua asiyependa kujua maana ya maono aliyoyaona au ndoto aliyoiota.Watu wote hupenda kujua ufafanuzi na maana halisi katika ndoto na maono.
MAONO na NDOTO huchanganya watu wengi hata kushindwa kuyatofautisha. Mtu aweza kuona maono fulani lakini akasema ameota ndoto.
 Au mtu anaweza kuota ndoto akasema ameona maono fulani.
Ndiposa Roho wa Bwana akanichukua na kunitaharakisha nifundishe MAONO na NDOTO.
Haleluya…
Sasa,
 Fungua moyo wako ili Bwana akakuhudumie kupitia fundisho hili.
Tuanze na andiko hili;
Itakuwa siku za mwisho,asema Mungu,nitawamwagia watu wote Roho yangu,na wana wenu na binti zenu watatabiri ; na vijana wenu wataona maono ; na wazee wenu wataota ndoto.” Matendo 2:17
Andiko tulilolisoma hivi sasa linatueleza namna gani itakavyokuwa ndani ya nyakati za mwisho.
 Mungu anasema wazi wazi kupitia kinywa cha mtume Petro.Anaanza kwa kusema atamwaga Roho yake kwa watu wote.
Tukio la kwanza baada ya Roho wa Mungu kuwashukia watu wake ni KUTABIRI.
 Em sema ,”  kutabiri. ”
Simply,neno kutabiri kibiblia lina maana ya kutoa unabii juu ya mambo yajayo kwa msaada wa nguvu za Roho mtakatifu.
 Yeye anayetabiri,hatabiri kwa nafsi yake, wala sio kwa mapenzi yake,Bali ni Roho mtakatifu ndiye yupo kazini akiwezesha utabiri kwa kinywa cha mtumishi wake.
Kupitia maandiko matakatifu,wapo watu kadha wa kadha waliopata kutabiri baada ya kushukiwa na nguvu za Roho mtakatifu.
Mfano;
 Tunasoma;
na roho ya Bwana itakujilia kwa nguvu,nawe utatabiri pamoja nao,nawe utageuzwa kuwa mtu mwingine .” 1 Samweli 10:6
Tukio la utabiri ni baada ya kujiliwa kwa nguvu na Roho ya Bwana,Kisha Biblia inaweka wazi kabisa ya kwamba yeye anayetabiri hubadilika na kuwa mtu mwingine.
 Kuwa mtu mwingine ni ile hali ya kuhama kwa uwezo wa kibinadamu katika kila hali,na uwezo wa Bwana kuchukua nafasi
 Maneno hayo ( 1 Samweli 10:6) anaambiwa Sauli mtu ambaye nabii Samweli alimpaka mafuta ya kiutumishi kwa kuongozwa na Mungu mwenyewe.
Sauli asingeliweza kutabiri kama asingelishukiwa na nguvu za Roho mtakatifu.Baada ya kujiliwa na nguvu za Mungu,Sauli akatabiri sawa sawa na neno la Mungu kupitia kinywa cha mtumishi wake Petro ( Matendo 2:17).
Mfano wa pili,ni huu;
 Unakumbuka
 Sauli alopomuasi BWANA MUNGU kwa kushindwa kutii sauti yake Mungu iliyomwambia aende kuwaangamiza Waamaleki wote,
 (1Samweli 15:1-23)
Baada ya dhambi ya kuasi,Biblia inasema ;
Basi,Roho ya Bwana ilikuwa imemuacha Sauli..’‘  1 Samweli 16:14
Ndiposa Sauli akaanza kumtafuta Daudi ili amuue.
 Sasa,
 Kuna kipindi ambacho Daudi alimkimbilia Samweli kujificha huko Rama ili kuiponya roho yake.Sauli akatuma kundi la kwanza kwenda kumkamata Daudi, kabla ya kundi la Sauli halijawakaribia wakina Daudi na kundi lao pamoja na Samweli aliyekuwa kiongozi wa kundi la akina Daudi.
Biblia inatuambia ;
 NGUVU ZIKAWAJILIA NAO WAKATABIRI,(Kundi la Sauli likatabiri).Vivyo hivyo naye Sauli akaamua kwenda yeye mwenyewe kumkamata Daudi;
 naye akatabili tena akavua nguo zake mbele ya Samweli,akalala uchi mchana kutwa na usiku kucha siku ile. ( 1 Samweli 19: 18-24).
Bwana Yesu asifiwe…
Haleluya….
Hivyo kutabiri ni udhihirisho wa nguvu za Mungu,Udhihilisho unaomfanya mtu wa rohoni kunena habari ya mambo yajayo anayo yaona katika ulimwengu wa roho.
Na hilo ndio tukio la kwanza baada ya Roho wa Mungu kumwagika kwa watu wake,tukio hilo la kwanza ni KUTABIRI.
Lakini Mungu hakuishia hapo,
 Anasema kwa kinywa cha Petro,kwamba baada ya kutabiri,
 vijana wakiume na wakike wataona MAONO.
 Tena Mungu hakuwaacha wazee.
 Kundi la wazee nalo halikusahaulika maana anasema;
“…wazee wenu wataota ndoto” Matendo 2:17
ITAENDELEA….
Usikose kabisa fundisho lijalo,ambapo tutaanza rasmi kuchimba kiundani juu ya MAONO,na tukimaliza tutaingia katika ufafanuzi wa kimaandiko kuhusu NDOTO.
*Ninakuomba usikose kabisa.
Kwa huduma ya maombi na maombezi,pamoja na huduma ya kukata shauli yaani huduma ya kuongozwa sala ya toba ili uokoke,piga namba hii;
 0655-111149
UBARIKIWE.
:)

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

SOMO:KUSIFU NA KUABUDU KATIKA BIBLIA.

HISTORIA YA MITUME WA YESU KRISTO NA VIFO VIFO